Share this page:  
 

Multilingual Scriptures

(Compare books in 2 different language versions of your choice)

Comparison Search:

Select Language version and font:
You can only select max. of two versions.
Book:
Chapter:
Verse:
---------
From: To:

Free Search:

Select Language version and font:
Enter search text:

Multilingual Scriptures Home » Swahili New Testament » Hebrews

Swahili New Testament
Chapter # Verse # Verse Detail
11Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii,
12lakini siku hizi za mwisho, amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu na akamteua avimiliki vitu vyote.
13Yeye ni mng`ao wa utukufu wa Mungu, na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akiutegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwapatia binadamu msamaha wa dhambi zao, aliketi huko juu mbinguni, upande wa kulia wa Mungu Mkuu.
14Mwana ni mkuu zaidi kuliko malaika, kama vile jina alilopewa na Mungu ni kuu zaidi kuliko jina lao.
15Maana Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: "Wewe ni Mwanangu; Mimi leo nimekuwa Baba yako." Wala hakusema juu ya malaika yeyote: "Mimi nitakuwa Baba yake, naye atakuwa Mwanangu."
16Lakini Mungu alipokuwa anamtuma Mwanae mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, alisema: "Malaika wote wa Mungu wanapaswa kumwabudu."
17Lakini kuhusu malaika, Mungu alisema: "Mungu awafanya malaika wake kuwa pepo, na watumishi wake kuwa ndimi za moto."
18Lakini kumhusu Mwana, Mungu alisema: "Utawala wako ee Mungu, wadumu milele na milele! Wewe wawatawala watu wako kwa haki.
19Wewe wapenda uadilifu na kuchukia uovu. Ndiyo maana Mungu, Mungu wako amekuweka wakfu na kukumiminia furaha kubwa zaidi kuliko wenzako."
110Pia alisema: "Bwana, wewe uliumba dunia hapo mwanzo, mbingu ni kazi ya mikono yako.
111Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki daima, zote zitachakaa kama vazi.
112Utazikunjakunja kama koti, nazo zitabadilishwa kama vazi. Lakini wewe ni yuleyule daima, na maisha yako hayatakoma."
113Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake: "Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako."
114Malaika ni roho tu wanaomtumikia Mungu, na Mungu huwatuma wawasaidie wale watakaopokea wokovu.
21Kwa sababu hiyo tunapaswa kuzingatia kwa makini zaidi yote tuliyosikia, ili tusije tukapotoshwa.
22Ujumbe ule waliopewa wazee wetu na malaika ulionyeshwa kuwa kweli, hata mtu yeyote ambaye hakuufuata au hakuutii aliadhibiwa kama alivyostahili.
23Basi, sisi tutaokokaje kama hatuujali wokovu mkuu kama huu? Kwanza Bwana mwenyewe aliutangaza wokovu huu, na wale waliomsikia walituthibitishia kwamba ni kweli.
24Mungu pia aliongeza hapo ushahidi wake kwa kufanya kila namna ya miujiza na maajabu, na kwa kuwagawia watu vipaji vya Roho Mtakatifu kadiri ya mapenzi yake.
25Mungu hakuwaweka malaika wautawale ulimwengu ujao, yaani ulimwengu ule tunaoongea habari zake.
26Tena yasemwa mahali fulani katika Maandiko: "Mtu ni nini ee Mungu, hata umfikirie; mwanaadamu ni nini hata umjali?
27Ulimfanya kwa kitambo kidogo kuwa chini zaidi kuliko malaika; ukamvika taji ya utukufu na heshima,
28ukaweka kila kitu chini ya miguu yake, avitawale." Yasemwa kwamba Mungu alimweka mtu kuwa mtawala wa vitu vyote yaani bila kuacha hata kimoja. Hata hivyo, hatuoni bado mtu akivitawala vitu vyote sasa.
29Lakini twamwona Yesu ambaye alifanywa kwa kitambo kidogo kuwa chini zaidi kuliko malaika, ili kwa neema ya Mungu afe kwa ajili ya watu wote. Sasa tunamwona ametawazwa kwa utukufu na heshima kwa sababu ya kifo alichoteseka.
210Ilikuwa haki tupu kwamba Mungu, ambaye huumba na kutegemeza vitu vyote, alimfanya Yesu kuwa mkamilifu kabisa kwa njia ya mateso, ili awalete watoto wengi waushiriki utukufu wake. Maana Yesu ndiye anayewaongoza kwenye wokovu.
211Yeye anawatakasa watu dhambi zao, naye pamoja na wale waliotakaswa, wote wanaye Baba mmoja. Ndiyo maana Yesu haoni aibu kuwaita hao ndugu zake;
212kama asemavyo: "Ee Mungu, nitawatangazia ndugu zangu matendo yako. Nitakusifu katika kusanyiko lao."
213Tena asema: "Nitamwekea Mungu tumaini langu." Na tena: "Mimi niko hapa pamoja na watoto alionipa Mungu."
214Basi, kwa vile watoto hao, kama awaitavyo, ni watu wenye mwili na damu, Yesu mwenyewe akawa kama wao na kushiriki ubinadamu wao. Alifanya hivyo ili kwa njia ya kifo chake amwangamize Ibilisi, ambaye ana mamlaka juu ya kifo,
215na hivyo awaokoe wale waliokuwa watumwa maisha yao yote kwa sababu ya hofu yao ya kifo.
216Maana ni wazi kwamba yeye hakuja kwa ajili ya kuwasaidia malaika, bali kama yasemavyo Maandiko; "Anawasaidia wazawa wa Abrahamu."
217Ndiyo maana ilimbidi awe kama ndugu zake kwa kila namna, ili awe Kuhani Mkuu wao aliye mwaminifu na mwenye huruma katika kumtumikia Mungu, ili dhambi za watu ziondolewe.
218Na, anaweza sasa kuwasaidia wale wanaojaribiwa na kuteswa.
31Ndugu zangu watu wa Mungu ambao mmeitwa na Mungu, fikirini juu ya Yesu ambaye Mungu alimtuma awe Kuhani Mkuu wa imani tunayoiungama.
32Yeye alikuwa mwaminifu kwa Mungu aliyemteua kufanya kazi yake kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu.
33Mjenzi wa nyumba hupata heshima zaidi kuliko hiyo nyumba yenyewe. Hali kadhalika naye Yesu anastahili heshima kubwa zaidi kuliko Mose.
34Kila nyumba hujengwa na mjenzi fulani--na Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote.
35Mose alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Bwana kama mtumishi, na alinena juu ya mambo ambayo Mungu atayasema hapo baadaye.
36Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana mwenye mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Sisi ni nyumba yake kama tukizingatia uhodari wetu na uthabiti wetu katika kile tunachotumainia.
37Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo,
38msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu; kama walivyokuwa siku ile kule jangwani,
39Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza, asema Bwana, ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu kwa miaka arobaini.
310Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema, `Fikira za watu hawa zimepotoka, hawajapata kamwe kuzijua njia zangu.`
311Basi, nilikasirika, nikaapa: `Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko."`
312Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai.
313Maadamu hiyo "Leo" inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi.
314Maana sisi tunashirikiana na Kristo ikiwa tutazingatia kwa uthabiti tumaini tulilokuwa nalo mwanzoni.
315Maandiko yasema hivi: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu kama wazee wenu walivyokuwa wakati walipomwasi Mungu."
316Ni akina nani basi, waliosikia sauti ya Mungu wakamwasi? Ni wale wote walioongozwa na Mose kutoka Misri.
317Mungu aliwakasirikia akina nani kwa miaka arobaini? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi, maiti zao zikatapakaa kule jangwani.
318Mungu alipoapa: "Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko," alikuwa anawasema akina nani? Alikuwa anasema juu ya hao walioasi.
319Basi, twaona kwamba hawakuingia huko kwa sababu hawakuamini.
41Mungu alituahidia kwamba tutaweza kupata pumziko hilo alilosema. Basi, na tuogope ili yeyote kati yenu asije akashindwa kupata pumziko hilo.
42Maana Habari Njema imehubiriwa kwetu kama vile ilivyohubiriwa kwa hao watu wa kale. Lakini ujumbe huo haukuwafaa chochote, maana waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani.
43Basi, sisi tunaoamini tunapata pumziko hilo aliloahidi Mungu. Kama alivyosema: "Nilikasirika, nikaapa: `Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko."` Mungu alisema hayo ingawa kazi yake ilikuwa imekwisha malizika tangu alipoumba ulimwengu.
44Maana Maandiko yasema mahali fulani kuhusu siku ya saba: "Mungu alipumzika siku ya saba, akaacha kazi zake zote."
45Tena jambo hili lasemwa pia: "Hawataingia huko ambako ningewapa pumziko."
46Wale waliotangulia kuhubiriwa Habari Njema hawakupata pumziko hilo kwa sababu hawakuamini. Wapo, basi, wengine ambao wangejaliwa kulipata.
47Jambo hili ni wazi, kwani Mungu aliweka siku nyingine ambayo inaitwa "Leo". Miaka mingi baadaye Mungu alisema juu ya hiyo siku kwa maneno ya Daudi katika Maandiko yaliyokwisha tajwa: "Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiifanye mioyo yenu kuwa migumu."
48Kama Yoshua angaliwapa watu hao hilo pumziko, Mungu hangalisema baadaye juu ya siku nyingine.
49Kwa hiyo, basi, bado lipo pumziko kwa watu wa Mungu kama kule kupumzika kwake Mungu siku ya saba.
410Maana, kila anayepata pumziko aliloahidi Mungu atapumzika baada ya kazi yake kama vile pia Mungu alivyopumzika baada ya yake.
411Basi, tujitahidi kupata pumziko hilo, ili asiwepo yeyote miongoni mwenu atakayeshindwa, kama walivyofanya wao kwa sababu ya ukosefu wao wa imani.
412Neno la Mungu ni hai na lina nguvu; ni kali zaidi kuliko upanga wenye makali kuwili. Hukata kabisa mpaka mahali ambapo moyo na roho hukutana, mpaka pale vikutanapo viungo vya mwili na mafuta. Neno hilo huchambua nia na fikira za mioyo ya watu.
413Hakuna kiumbe chochote kilichofichika mbele ya Mungu; kila kitu kimefunuliwa wazi mbele ya macho yake. Kwake, sisi sote tutapaswa kutoa hoja ya matendo yetu.
414Basi, tunapaswa kuzingatia kwa uthabiti imani tunayoiungama. Maana tunaye Kuhani Mkuu aliyeingia mpaka kwa Mungu mwenyewe--Yesu, Mwana wa Mungu.
415Huyu Kuhani Mkuu wetu si mmoja ambaye hawezi kutuunga mkono katika unyonge wetu, ila ni Kuhani Mkuu ambaye alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda dhambi.
416Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu, palipo na neema, ili tukajipatie huruma na neema ya kutusaidia wakati wa lazima.
51Kila kuhani mkuu huchaguliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya kumtumikia Mungu kwa niaba yao, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi zao.
52Maadamu yeye mwenyewe yu dhaifu anaweza kuwaonea huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa.
53Na kwa vile yeye mwenyewe ni dhaifu, anapaswa kutolea dhabihu si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake.
54Hakuna mtu awezaye kujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni.
55Hali kadhalika naye Kristo hakujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu, bali Mungu alimwambia: "Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa baba yako."
56Alisema pia mahali pengine: "Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."
57Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka kifo; naye alisikilizwa kwa sababu ya kumcha Mungu.
58Lakini, ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kutii kwa njia ya mateso.
59Na alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wale wote wanaomtii,
510naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.
511Tunayo Mengi ya kusema juu ya jambo hili, lakini ni vigumu kuwaelezeni, kwa sababu ninyi si wepesi wa kuelewa.
512Sasa mngalipaswa kuwa tayari walimu, lakini mnahitaji bado mtu wa kuwafundisheni mafundisho ya mwanzo ya ujumbe wa Mungu. Badala ya kula chakula kigumu, mnapaswa bado kunywa maziwa.
513Kila anayepaswa kunywa maziwa huyo ni mtoto bado, hajui uadilifu ni nini.
514Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu waliokomaa, ambao wanaweza kubainisha mema na mabaya.
61Basi, tusonge mbele kwa yale yaliyokomaa na kuyaacha nyuma yale mafundisho ya mwanzo ya Kikristo. Hatuhitaji kuweka msingi tena kwa kurudia yale mafundisho ya mwanzo kama vile kuachana na matendo ya kifo, kumwamini Mungu;
62mafundisho juu ya ubatizo na kuwekewa mikono; ufufuo wa wafu na hukumu ya milele.
63tusonge mbele! Hayo tutayafanya, Mungu akitujalia.
64Maana watu wanaoiasi imani yao inawezekanaje kuwarudisha watubu tena? Watu hao walikwisha kuwa katika mwanga wa Mungu, walikwisha onja zawadi ya mbinguni na kushirikishwa Roho Mtakatifu;
65walikwisha onja wema wa neno la Mungu na nguvu za ulimwengu ujao,
66kisha wakaiasi imani yao! Haiwezekani kuwarudisha watubu tena, kwa sababu wanamsulubisha tena Mwana wa Mungu na kumwaibisha hadharani.
67Mungu huibariki ardhi ambayo huipokea mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuotesha mimea ya faida kwa mkulima.
68Lakini kama ardhi hiyo ikiota miti ya miiba na magugu, haina faida; karibu italaaniwa na Mungu na mwisho wake ni kuchomwa moto.
69Lakini, ingawa twasema namna hii, wapenzi wetu, tunalo tumaini kubwa juu ya hali yenu. Tunajua kwamba mmepokea baraka zile bora za wokovu wenu.
610Mungu hakosi haki; yeye hataisahau kazi mliyoifanya au upendo mlioonyesha kwa ajili ya jina lake katika huduma mliyowapa na mnayowapa sasa watu wake.
611Hamu yetu ni kwamba kila mmoja wenu aonyeshe bidii hiyohiyo mpaka mwisho, ili yale mnayotumainia yapate kutimia.
612Msiwe wavivu, bali muwe kama wale wanaoamini na wenye uvumilivu na hivyo wanapokea yake aliyoahidi Mungu.
613Mungu alipompa Abrahamu ahadi, aliapa kwa jina lake mwenyewe, maana hakuna aliye mkuu kuliko Mungu ambaye kwa huyo angeweza kuapa.
614Mungu alisema: "Hakika nitakubariki na nitakupa wazawa wengi."
615Abrahamu alisubiri kwa uvumilivu na hivyo alipokea kile alichoahidiwa na Mungu.
616Watu wanapoapa, huapa kwa mmoja aliye mkuu zaidi kuliko wao, na kiapo hicho husuluhisha ubishi wote.
617Naye Mungu aliimarisha ahadi yake kwa kiapo; na kwa namna hiyo akawaonyesha wazi wale aliowaahidia kwamba hatabadili nia yake.
618Basi, kuna vitu hivi viwili: ahadi na kiapo, ambavyo haviwezi kubadilika na wala juu ya hivyo Mungu hawezi kusema uongo. Kwa hiyo sisi tuliokimbilia usalama kwake, tunapewa moyo wa kushikilia imara tumaini lililowekwa mbele yetu.
619Tunalo tumaini hilo kama nanga ya maisha yetu. Tumaini hilo ni imara na thabiti, nalo lapenya lile pazia la hekalu la mbinguni mpaka patakatifu ndani.
620Yesu ametangulia kuingia humo kwa niaba yetu, na amekuwa kuhani mkuu milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.
71Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu, na kuhani wa Mungu Mkuu. Abrahamu alipokuwa anarudi kutoka vitani ambako aliwaua wafalme, Melkisedeki alikutana naye akambariki,
72naye Abrahamu akampa sehemu ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. (Maana ya kwanza ya jina hili Melkisedeki ni "Mfalme wa Uadilifu"; na, kwa vile yeye alikuwa mfalme wa Salemu, jina lake pia lina maana ya "Mfalme wa Amani.")
73Baba yake na mama yake hawatajwi, wala ukoo wake hautajwi; haisemwi alizaliwa lini au alikufa lini. Anafanana na Mwana wa Mungu, na anaendelea kuwa kuhani daima.
74Basi, mwaona jinsi mtu huyu alivyokuwa maarufu. Baba Abrahamu alimpa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyoteka vitani.
75Tunajua vilevile kwamba kufuatana na Sheria, wana wa Lawi ambao ni makuhani, wanayo haki ya kuchukua sehemu ya kumi kutoka kwa watu, yaani ndugu zao, ingawaje nao ni watoto wa Abrahamu.
76Lakini huyo Melkisedeki hakuwa wa ukoo wa Lawi, hata hivyo alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu; tena akambariki yeye ambaye alikuwa amepewa ahadi ya Mungu.
77Hakuna mashaka hata kidogo kwamba anayebariki ni mkuu zaidi kuliko yule anayebarikiwa.
78Tena, hao makuhani wanaopokea sehemu ya kumi, ni watu ambao hufa; lakini hapa anayepokea sehemu ya kumi, yaani Melkisedeki, anasemekana kwamba hafi.
79Twaweza, basi, kusema kwamba Abrahamu alipotoa sehemu moja ya kumi, Lawi (ambaye watoto wake hupokea sehemu moja ya kumi) alitoa sehemu moja ya kumi pia.
710Maana Lawi hakuwa amezaliwa bado, bali ni kama alikuwa katika mwili wa baba yake, Abrahamu, wakati Melkisedeki alipokutana naye.
711Kutokana na ukuhani wa Walawi, watu wa Israeli walipewa Sheria. Sasa, kama huduma ya Walawi ingalikuwa kamilifu hapangekuwa tena na haja ya kutokea ukuhani mwingine tofauti, ukuhani ambao umefuata utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki, na si ule wa Aroni.
712Maana ukuhani ukibadilika ni lazima Sheria nayo ibadilike.
713Naye Bwana wetu ambaye mambo hayo yote yanasemwa juu yake, alikuwa wa kabila lingine, na wala hakuna hata mmoja wa kabila lake aliyepata kutumikia madhabahuni akiwa kuhani.
714Inafahamika wazi kwamba yeye alizaliwa katika kabila la Yuda ambalo Mose hakulitaja alipokuwa anasema juu ya makuhani.
715Tena jambo hili ni dhahiri zaidi: kuhani mwingine anayefanana na Melkisedeki amekwisha tokea.
716Yeye hakufanywa kuwa kuhani kwa sheria na maagizo ya kibinadamu, bali kwa nguvu ya uhai ambao hauna mwisho.
717Maana Maandiko yasema: "Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."
718Basi, ile amri ya zamani ilifutwa kwa sababu ilikuwa hafifu na isiyofaa kitu.
719Maana Sheria ya Mose haikuweza kukamilisha jambo lolote. Lakini sasa, mahali pake pamewekwa tumaini lililo bora zaidi ambalo kwalo tunaweza kumkaribia Mungu.
720Zaidi ya hayo hapa pana kiapo cha Mungu. Wakati wale wengine walipofanywa makuhani hapakuwako kiapo.
721Lakini Yesu alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alipomwambia: "Bwana ameapa, wala hataigeuza nia yake: `Wewe ni kuhani milele."`
722Basi, kutokana na tofauti hii, Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.
723Kuna tofauti nyingine pia: hao makuhani wengine walikuwa wengi kwa sababu walikufa na hawakuweza kuendelea na kazi yao.
724Lakini Yesu si kama wao, yeye anaishi milele; ukuhani wake hauondoki kwake.
725Hivyo, yeye anaweza daima kuwaokoa kabisa wote wanaomwendea Mungu kwa njia yake, maana yeye anaishi milele kuwaombea kwa Mungu.
726Basi, Yesu ndiye Kuhani Mkuu ambaye anatufaa sana katika mahitaji yetu. Yeye ni mtakatifu, hana hatia wala dhambi ndani yake; hayumo katika kundi la wenye dhambi na ameinuliwa mpaka juu mbinguni.
727Yeye si kama wale makuhani wakuu wengine; hana haja ya kutoa dhabihu kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Yeye alifanya hivyo mara moja tu wakati alipojitoa yeye mwenyewe, na hiyo yatosha kwa nyakati zote.
728Sheria ya Mose huwateua watu waliokuwa dhaifu kuwa makuhani wakuu; lakini ahadi ya Mungu aliyoifanya kwa kiapo na ambayo imefika baada ya sheria imemteua Mwana ambaye amefanywa mkamilifu milele.
81Basi, jambo muhimu katika hayo tunayosema ni hili: sisi tunaye Kuhani Mkuu wa namna hiyo, ambaye anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu mbinguni.
82Yeye hutoa huduma ya Kuhani Mkuu katika Mahali Patakatifu sana, yaani ndani ya ile hema ya kweli iliyojengwa na Bwana, siyo na binadamu. ic
83Kila Kuhani Mkuu ameteuliwa kumtolea Mungu vipawa na dhabihu, na hivyo Kuhani Mkuu wetu lazima pia awe na kitu cha kutolea.
84Kama yeye angekuwa wa hapa duninani, asingekuwa kamwe kuhani, kwani wako makuhani wengine wanaotoa sadaka kufuatana na Sheria.
85Huduma zao za kikuhani ni mfano tu na kivuli cha yale yaliyoko mbinguni. Ndivyo pia ilivyokuwa kwa Mose. Wakati alipokuwa karibu kuitengeneza ile hema, Mungu alimwambia: "Tengeneza kila kitu kufuatana na ule mfano ulioonyeshwa kule mlimani."
86Lakini sasa Yesu amepewa huduma ya kikuhani iliyo bora zaidi kuliko yao, kama vile agano alilothibitisha kati ya watu na Mungu ni bora zaidi, kwani lina msingi wake katika ahadi za mambo yaliyo bora zaidi.
87Maana kama lile agano la kwanza halingalikuwa na dosari, hakungalikuwa na haja ya agano la pili.
88Lakini Mungu aliwalaumu watu wake aliposema: "Siku zinakuja, asema Bwana, ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na kabila la Yuda.
89Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na babu zao siku ile nilipowaongoza kwa mkono kutoka nchi ya Misri. Hawakuwa waaminifu kwa agano langu; na hivyo mimi sikuwajali, asema Bwana.
810Na hili ndilo agano nitakalofanya na watu wa Israeli siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu akilini mwao, na kuziandika mioyoni mwao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
811Hakuna mtu atakayemfundisha mwananchi mwenzake, wala atakayemwambia ndugu yake: `Mjue Bwana.` Maana watu wote, wadogo na wakubwa, watanijua mimi.
812Nitawasamehe makosa yao, wala sitakumbuka tena dhambi zao."
813Kwa kusema juu ya agano jipya, Mungu alilichakaza lile la kwanza; na chochote kinachochakaa na kuwa kikuukuu kitatoweka karibuni.
91Agano la kwanza lilikuwa na taratibu zake za ibada na pia mahali patakatifu pa ibada palipojengwa na watu.
92Palitengenezwa hema ambayo sehemu yake ya nje iliitwa Mahali Patakatifu. Humo mlikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyotolewa kwa Mungu.
93Nyuma ya pazia la pili, kulikuwa na hema iliyoitwa Mahali Patakatifu Kupita Pote.
94Humo mlikuwa na madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kufukizia ubani, na Sanduku la Agano, ambalo lilikuwa limepakwa dhahabu pande zote, na ndani yake mlikuwa na chungu cha dhahabu kilichokuwa na mana; fimbo ya Aroni iliyokuwa imechanua majani, na vile vibao viwili vilivyoandikwa agano.
95Juu ya hilo Sanduku kulikuwa na viumbe vilivyodhihirisha kuweko kwa Mungu, na mabawa yao yalitanda juu ya mahali ambapo dhambi huondolewa. Lakini sasa, hatuwezi kusema kinaganaga juu ya mambo hayo.
96Mipango hiyo ilitekelezwa kisha ikawa desturi kwa makuhani kuingia kila siku katika hema ya nje kutoa huduma zao.
97Lakini kuhani Mkuu peke yake ndiye anayeingia katika lile hema la pili; naye hufanya hivyo mara moja tu kwa mwaka. Anapoingia ndani huwa amechukua damu ambayo anamtolea Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi ambazo watu wamezitenda bila wao wenyewe kujua.
98Kutokana na taratibu hizo Roho Mtakatifu anafundisha wazi kwamba wakati ile hema ya nje ingali ipo imesimama, njia ya kuingia Mahali Patakatifu haijafunguliwa.
99Jambo hili ni mfano wa nyakati za sasa. Linaonyesha kwamba zawadi na dhabihu zinazotolewa kwa Mungu haziwezi kuifanya mioyo ya wale wanaoabudu kuwa mikamilifu,
910kwani haya yote yanahusika na vyakula, vinywaji na taratibu mbalimbali za kutawadha. Yote hayo ni maagizo ya njenje tu; na nguvu yake hukoma wakati Mungu atakaporekebisha vitu vyote.
911Lakini Kristo amekwisha fika, akiwa Kuhani Mkuu wa mambo yaliyo mema, ambayo sasa yamekwisha fika. Yeye anatoa huduma zake katika hema iliyo bora na kamilifu zaidi, isiyofanywa kwa mikono ya watu, yaani isiyo ya ulimwengu huu ulioumbwa.
912Yeye aliingia Mahali Patakatifu mara moja tu, tena hakuwa amechukua damu ya mbuzi wala ng`ombe, bali aliingia kwa damu yake yeye mwenyewe, akatupatia ukombozi wa milele.
913Watu waliokuwa najisi kidini waliweza kutakasika na kuwa safi waliponyunyiziwa damu ya mbuzi na ya ng`ombe pamoja na majivu ya ndama.
914Lakini, kwa damu ya Kristo, mambo makuu zaidi hufanyika! Kwa nguvu za Roho wa milele, Kristo alijitolea mwenyewe dhabihu kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo kifo, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai.
915Kwa hiyo, Kristo ndiye aliyeratibisha agano jipya ili wale walioitwa na Mungu wazipokee baraka za milele walizoahidiwa. Watazipata, kwani kifo kimetokea ambacho huwakomboa watu kutoka yale makosa waliyofanya wakati wa lile agano la kale.
916Kwa kawaida wosia hutambuliwa tu kama kifo cha yule aliyeufanya huo wosia kimethibitishwa.
917Wosia hauwezi kutekelezwa mpaka kumetokea kifo, kwani wosia hauna maana ikiwa mwenye kuufanya bado anaishi.
918Ndiyo maana hata lile agano la kwanza halikuwekwa bila damu kumwagwa.
919Kwanza Mose aliwatangazia watu wote amri zote kama ilivyokuwa katika Sheria; kisha akachukua damu ya ndama pamoja na maji, na kwa kutumia majani ya mti uitwao husopo na pamba nyekundu, akakinyunyizia kile kitabu cha Sheria na hao watu wote.
920Mose alisema: "Hii ni damu inayothibitisha agano mliloamriwa na Mungu mlitii."
921Vilevile Mose aliinyunyizia damu ile hema na vyombo vya ibada.
922Naam, kadiri ya Sheria karibu kila kitu chaweza kutakaswa kwa damu, na dhambi nazo zaondolewa tu ikiwa damu imemwagwa.
923Vitu hivi ambavyo ni mfano tu wa mambo halisi ya mbinguni, vililazimika kutakaswa kwa namna hiyo. Lakini vitu vya mbinguni huhitaji dhabihu iliyo bora zaidi.
924Maana Kristo hakuingia Mahali Patakatifu palipojengwa kwa mikono ya watu, ambapo ni mfano tu wa kile kilicho halisi. yeye aliingia mbinguni kwenyewe ambako sasa anasimama mbele ya Mungu kwa ajili yetu.
925Kuhani Mkuu wa Wayahudi huingia Mahali Patakatifu kila mwaka akiwa amechukua damu ya mnyama; lakini Kristo hakuingia humo ili ajitoe mwenyewe mara nyingi,
926maana ingalikuwa hivyo, Kristo angalipaswa kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa ulimwengu. Lakini sasa nyakati hizi zinapokaribia mwisho wake, yeye ametokea mara moja tu, kuondoa dhambi kwa kujitoa yeye mwenyewe dhabihu.
927Basi, kama vile kila mtu hufa mara moja tu, kisha husimama mbele ya hukumu ya Mungu,
928vivyo hivyo Kristo naye alijitoa dhabihu mara moja tu kwa ajili ya kuziondoa dhambi za wengi. Atakapotokea mara ya pili si kwa ajili ya kupambana na dhambi, bali ni kwa ajili ya kuwaokoa wale wanaomngojea.
101Sheria ya Wayahudi si picha kamili ya mambo yale halisi: ni kivuli tu cha mema yanayokuja. Dhabihu zilezile hutolewa daima, mwaka baada ya mwaka. Sheria yawezaje, basi, kwa njia ya dhabihu hizo, kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu?
102Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na dhabihu hizo zote zingekoma.
103Lakini dhabihu hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao.
104Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi.
105Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: "Hukutaka dhabihu wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili.
106Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi.
107Hapo nikasema: `Niko hapa ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha Sheria."`
108Kwanza alisema: "Hutaki, wala hupendezwi na dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi." Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na Sheria.
109Kisha akasema: "Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako." Hivyo Mungu alibatilisha dhabihu za zamani na mahali pake akaweka dhabihu nyingine moja.
1010Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza mapenzi ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile dhabihu ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha.
1011Kila kuhani Myahudi humhudumia Mungu kila siku, akitoa dhabibu zilezile mara nyingi, dhabibu ambazo haziwezi kuondoa dhambi.
1012Lakini Kristo alitoa dhabihu moja tu kwa ajili ya dhambi, dhabihu ifaayo milele, kisha akaketi upande wa kulia wa Mungu.
1013Huko anangoja mpaka adui zake watakapowekwa kama kibao chini ya miguu yake.
1014Basi, kwa dhabihu yake moja tu, amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wanaotakaswa dhambi zao.
1015Naye Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema:
1016"Hili ndilo agano nitakalofanya nao, katika siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao."
1017Kisha akaongeza kusema: "Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu."
1018Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa dhabihu za kuondoa dhambi.
1019Basi, ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu.
1020Yeye ametufungulia njia mpya na yenye uzima kupitia lile pazia, yaani kwa njia ya mwili wake mwenyewe.
1021Basi, tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu.
1022Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi.
1023Tushikilie imara tumaini lile tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
1024Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema.
1025Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, Siku ile ya Bwana inakaribia.
1026Maana, tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kufahamu ukweli, hakuna dhabihu iwezayo kutolewa tena kwa ajili ya kuondoa dhambi.
1027Linalobaki ni kungojea tu kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali utakaowaangamiza wote wanaompinga.
1028Mtu yeyote asiyeitii Sheria ya Mose, huuawa bila ya huruma kukiwa na ushahidi wa watu wawili au watatu.
1029Je, mtu yule anayempuuza Mwana wa Mungu na kuidharau damu ya agano la Mungu iliyomtakasa, mtu anayemtukana Roho wa Mungu, anastahili kupata adhabu kali ya namna gani?
1030Maana tunamfahamu yule aliyesema, "Mimi nitalipiza kisasi, mimi nitalipiza," na ambaye alisema pia, "Bwana atawahukumu watu wake."
1031Kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai ni jambo la kutisha mno!
1032Kumbukeni yaliyotokea siku zile za kwanza mlipoangaziwa mwanga wa Mungu. Ingawa siku zile mlipatwa na mateso mengi, ninyi mlistahimili.
1033Mara nyingine mlitukanwa na kufedheheshwa hadharani; mara nyingine mlikuwa radhi kuungana na wale walioteswa namna hiyohiyo.
1034Mlishiriki mateso ya wafungwa, na mliponyang`anywa mali yenu mlistahimili kwa furaha, maana mlijua kwamba mnayo mali bora zaidi na ya kudumu milele.
1035Basi, msipoteze uhodari wenu, maana utawapatieni tuzo kubwa.
1036Mnahitaji kuwa na uvumilivu, ili mweze kufanya anayotaka Mungu na kupokea kile alichoahidi.
1037Maana kama yasemavyo Maandiko: "Bado kidogo tu, na yule anayekuja, atakuja, wala hatakawia.
1038Lakini mtu wangu aliye mwadilifu ataamini na kuishi; walakini akirudi nyuma, mimi sitapendezwa naye."
1039Basi, sisi hatumo miongoni mwa wale wanaorudi nyuma na kupotea, ila sisi tunaamini na tunaokolewa.
111Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona.
112Maana wazee wa kale walipata kibali cha Mungu kwa sababu ya imani yao.
113Kwa imani sisi tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu; vitu vinavyoonekana kutoka vitu visivyoonekana.
114Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu iliyokuwa bora zaidi kuliko ile ya Kaini. Kwa imani yake alikubaliwa na Mungu kuwa mwadilifu; Mungu mwenyewe alizikubali sadaka zake. Kwa imani yake ingawa amekufa, bado ananena.
115Kwa imani Henoki alichukuliwa na Mungu, asipate kufa. Hakuonekana tena kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Maandiko yasema kwamba kabla ya kuchukuliwa kwake, yeye alikuwa amempendeza Mungu.
116Basi, pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Kwa maana kila mtu anayemwendea Mungu ni lazima aamini kwamba Mungu yuko, na kwamba huwatuza wale wanaomtafuta.
117Kwa imani Noa alionywa na Mungu juu ya mambo ya baadaye ambayo hakuweza kuyaona bado. Alimtii Mungu, akajenga ile safina ambamo aliokolewa yeye pamoja na jamaa yake. Kutokana na hayo ulimwengu ulihukumiwa, naye Noa akapokea uadilifu unaotokana na imani.
118Kwa imani Abrahamu alimtii Mungu alipoitwa aende katika nchi ambayo Mungu angempa iwe yake. Ingawa hakujua alikokuwa anakwenda, Abrahamu alihama.
119Kwa imani aliishi kama mgeni katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Aliishi huko katika hema kama walivyoishi Isaka na Yakobo, ambao pia walishiriki ahadi ileile.
1110Maana Abrahamu alikuwa akingojea mji wenye misingi imara, mji ambao Mungu mwenyewe ndiye fundi aliyeubuni na kuujenga.
1111Kwa imani hata Sara aliamini kwamba Mungu hutimiza ahadi zake, kwa hiyo akajaliwa kuchukua mimba ingawaje alikuwa amepita umri.
1112Kwa hiyo, kutoka katika mtu huyo mmoja, Abrahamu, ambaye alikuwa kama amekufa, walitokea watu wengi wasiohesabika kama vile nyota za mbinguni na mchanga wa pwani.
1113Watu hawa wote walikufa wakiwa na imani. Walikufa kabla ya kupokea mambo ambayo Mungu alikuwa ameahidi, lakini kwa mbali waliyaona, wakashangilia, na kukiri wazi kwamba wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani.
1114Watu wanaosema mambo kama hayo, huonyesha wazi kwamba wanaitafuta nchi yao wenyewe.
1115Kama wangalikuwa wanaifikiria nchi walikotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko.
1116Lakini sasa wanataka nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Ndiyo maana Mungu haoni haya wakimwita yeye Mungu wao, kwa sababu yeye mwenyewe amekwisha watayarishia mji.
1117Kwa imani, Abrahamu alimtoa mwanae Isaka sadaka wakati Mungu alipomjaribu. Huyo Abrahamu ndiye aliyekuwa amepokea ahadi ya Mungu, lakini, hata hivyo, alikubali kumtoa dhabihu mwanae wa pekee,
1118ingawa Mungu alikuwa amemwambia: "Wazawa wako watatokana na Isaka."
1119Abrahamu aliamini kwamba Mungu anaweza kuwafufua wafu: na kwa namna fulani kweli Abrahamu alimpata tena mwanae kutoka wafu.
1120Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau, wapate baraka zitakazokuja baadaye.
1121Kwa imani Yakobo alipokuwa karibu kufa, aliwabariki kila mmoja wa wana wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiegemea ile fimbo yake.
1122Kwa imani Yosefu alipokuwa karibu kufa, alinena juu ya kutoka kwa Waisraeli katika nchi ya Misri, na pia akawaachia maagizo kuhusu mifupa yake.
1123Kwa imani wazazi wa Mose walimficha huyo mtoto kwa muda wa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Walimwona kuwa ni mtoto mzuri, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.
1124Kwa imani Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao.
1125Aliona ni afadhali kuteseka pamoja na watu wa Mungu kuliko kufurahia raha ya dhambi kwa kitambo kidogo.
1126Alitambua kwamba kuteseka kwa ajili ya Masiha kuna faida kubwa zaidi kuliko utajiri wote wa nchi ya Misri, maana alikuwa anatazamia tuzo la baadaye.
1127Kwa imani Mose alihama kutoka nchi ya Misri bila kuogopa hasira ya mfalme; na wala hakurudi nyuma, kwani alikuwa kama mtu aliyemwona yule Mungu asiyeonekana.
1128Kwa imani aliadhimisha siku ya Pasaka, akaamuru damu inyunyizwe juu ya milango, ili yule Malaika Mwangamizi asiwaue wazaliwa wa kwanza wa Israeli.
1129Kwa imani watu wa Israeli walivuka bahari ya Shamu, kana kwamba ilikuwa nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo walikufa maji.
1130Kwa imani kuta za mji wa Yeriko zilianguka watu wa Israeli walipokwisha zunguka kwa muda wa siku saba.
1131Kwa imani Rahabu aliyekuwa malaya hakuangamia pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa sababu aliwakaribisha wale wapelelezi.
1132Basi, niseme nini zaidi? Wakati hauniruhusu kueleza juu ya Gedeoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii.
1133Kwa imani hawa wote walipigana vita na wafalme, wakashinda. Walitenda mambo adili, wakapokea yale aliyoahidi Mungu. Walifunga vinywa vya simba,
1134Walizima mioto mikali, waliepuka kuuawa kwa upanga. Walikuwa dhaifu lakini walipata nguvu. Walikuwa hodari katika vita wakashinda majeshi ya kigeni.
1135Na, wanawake walioamini walirudishiwa wafu wao wakiwa wamefufuliwa. Baadhi yao walikataa kufunguliwa, wakateswa mpaka kufa ili wapate kufufuliwa na kuingia katika maisha bora zaidi.
1136Wengine walidhihakiwa na kupigwa mijeledi, na wengine walifungwa minyororo na kutupwa gerezani.
1137Walipigwa mawe, walipasuliwa vipandevipande, waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi, walikuwa watu maskini, walioteswa na kudhulumiwa.
1138Ulimwengu haukustahili kuwa na watu hao. Walitangatanga jangwani na mlimani, wakaishi katika mashimo na mapango ya ardhi.
1139Watu hawa wote walionekana kuwa mashujaa kwa sababu ya imani yao. Hata hivyo, hawakupokea yale ambayo Mungu aliwaahidia,
1140maana Mungu alikuwa ameazimia mpango ulio bora zaidi kwa ajili yetu; yaani wao wangeufikia ukamilifu wakiwa pamoja nasi.
121Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotung`ang`ania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu.
122Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kujali juu ya aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.
123Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala msikate tamaa.
124Maana katika kupambana na dhambi, ninyi hamjapigana mpaka kiasi cha kumwaga damu yenu.
125Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu anawataja ninyi kuwa wanawe? "Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usife moyo anapokukanya.
126Maana Bwana humwadhibu kila anayempenda, humpinga kila anayekubali kuwa mwanae."
127Vumilieni adhabu kwani ni mafundisho; Mungu huwatendea ninyi kama wanawe. Maana ni mwana gani asiyeadhibiwa na baba yake?
128Lakini msipoadhibiwa kama wana wengine, basi, ninyi si wanawe, bali ni wana haramu.
129Zaidi ya hayo sisi tunawaheshimu wazazi wetu waliotuzaa hata wanapotuadhibu. Basi, tunapaswa kumtii zaidi Baba yetu wa kiroho ili tupate kuishi.
1210Wazazi wetu hapa duniani walituadhibu kwa muda, kama wao wenyewe walivyoona kuwa vema; lakini Mungu anatuadhibu kwa ajili ya faida yetu wenyewe, tupate kuushiriki utakatifu wake.
1211Kuadhibiwa si jambo la kufurahisha bali la kuhuzunisha. Lakini wale waliofunzwa kuwa na nidhamu mwishowe watavuna tuzo la amani kutoka katika maisha adili!
1212Basi, inueni mikono yenu inayolegea na kuimarisha magoti yenu yaliyo dhaifu.
1213Endeleeni kutembea katika njia iliyonyoka, ili kile kilicholemaa kisiumizwe, bali kiponywe.
1214Jitahidini kuishi kwa amani na watu wote. Ishini maisha ya utakatifu, kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Bwana bila ya maisha kama hayo.
1215Jitahidini sana mtu yeyote asije akapoteza neema ya Mungu. Muwe waangalifu ili mti mchungu usizuke kati yenu na kuwaua wengi kwa sumu yake.
1216Jihadharini ili miongoni mwenu pasiwe na mtu mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, aliyeuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa mlo mmoja.
1217Ninyi mnafahamu kwamba hata alipotaka kuipata tena ile baraka iliyokuwa yake, alikataliwa, maana hakupata tena nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.
1218Ninyi hamkuwasili mlimani Sinai, ambao unaweza kushikika kama walivyofanya watu wa Israeli, hamkufika kwenye moto uwakao, penye giza, tufani,
1219mvumo wa tarumbeta na sauti ya maneno. Wale waliosikia sauti hiyo waliomba wasisikie tena neno jingine,
1220kwani hawakuweza kustahimili amri iliyotolewa: "Atakayegusa mlima huu, hata kama ni mnyama, atapigwa mawe."
1221Hayo yote yalionekana ya kutisha mno, hata Mose akasema, "Naogopa na kutetemeka."
1222Lakini ninyi mmefika katika mlima wa Sioni, kwenye mji wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa mbinguni, ambapo wamekusanyika malaika elfu nyingi wasiohesabika.
1223Mmefika kwenye kusanyiko kubwa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mnasimama mbele ya Mungu aliye hakimu wa wote, na mbele ya roho za watu waadilifu waliofanywa kuwa wakamilifu.
1224Mmefika kwa Yesu ambaye ameratibisha agano jipya, na ambaye damu yake iliyomwagika inasema mambo mema zaidi kuliko ile ya Abeli.
1225Basi, jihadharini msije mkakataa kumsikiliza yeye ambaye anasema nanyi. Kama wale walikataa kumsikiliza yule aliyewaonya hapa duniani hawakuokoka, sisi tutawezaje kuokoka kama tukikataa kumsikiliza yule anayetuonya kutoka mbinguni?
1226Wakati ule sauti ilitetemesha nchi, lakini sasa ameahidi: "Nitatetemesha nchi tena, lakini si nchi tu bali pia mbingu."
1227Neno hili: "tena" linatuonyesha kwamba vitu vyote vilivyoumbwa vitatetemeshwa na kutoweka ili vibaki vile visivyotetemeshwa.
1228Sisi basi, na tushukuru kwani tunapokea utawala usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu;
1229maana Mungu wetu kweli ni moto mkali unaoteketeza.
131Endeleeni kupendana kidugu.
132Msisahau kuwakaribisha wageni; maana kwa kufanya hivyo watu wengine walipata kuwakaribisha malaika bila kujua.
133Wakumbukeni wale waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao. Wakumbukeni wale wanaoteseka kana kwamba nanyi mnateseka kama wao.
134Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote, na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu. Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi.
135Msiwe watu wa kupenda fedha; toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: "Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa."
136Ndiyo maana tunathubutu kusema: "Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?"
137wakumbukeni viongozi wenu waliowatangazieni ujumbe wa Mungu. Fikirieni juu ya mwenendo wao, mkaige imani yao.
138Yesu Kristo ni yuleyule, jana, leo na milele.
139Msipeperushwe huku na huku kwa mafundisho tofauti ya kigeni. Neema ya Mungu ndiyo inayoimarisha roho zetu na wala si masharti juu ya chakula; masharti hayo hayakumsaidia kamwe mtu yeyote aliyeyafuata.
1310Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaotumikia bado katika hema la Wayahudi, hawana haki ya kula vitu vyake.
1311Kuhani Mkuu wa Kiyahudi huleta damu ya wanyama katika Mahali Patakatifu na kuitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi; lakini nyama za hao wanyama huteketezwa nje ya kambi.
1312Ndiyo maana Yesu pia, kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa na kufa nje ya mji.
1313Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake.
1314Maana hapa duniani hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja.
1315Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa na midomo inayoliungama jina lake.
1316Msisahau kutenda mema na kusaidiana, maana hizi ndizo dhabihu zinazompendeza Mungu.
1317Watiini viongozi wenu na kushika amri zao; wao huchunga roho zenu usiku na mchana, na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu. Kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha, la sivyo, watazifanya kwa huzuni, na hiyo haitakuwa na faida kwenu.
1318Tuombeeni na sisi. Tuna hakika kwamba tunayo dhamiri safi, maana twataka kufanya lililo sawa daima.
1319Nawasihi sana mniombee ili Mungu anirudishe kwenu upesi iwezekanavyo.
1320Mungu amemfufua Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni Mchungaji Mkuu wa kondoo kwa sababu ya kumwaga damu yake iliyothibitisha agano la milele.
1321Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze mapenzi yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina.
1322Basi, ndugu, nawasihi mpokee kwa utulivu ujumbe huu wa kuwatieni moyo. Hii ni barua fupi tu ambayo nimewaandikieni.
1323Napenda kuwajulisheni kwamba ndugu yetu Timotheo amekwisha funguliwa gerezani. Kama akifika hapa mapema, nitakuja naye nitakapokuja kwenu.
1324Wasalimieni viongozi wenu wote pamoja na watu wa Mungu! Ndugu wa Italia wanawasalimuni.
1325Tunawatakieni nyote neema ya Mungu.