Share this page:  
 

Multilingual Scriptures

(Compare books in 2 different language versions of your choice)

Comparison Search:

Select Language version and font:
You can only select max. of two versions.
Book:
Chapter:
Verse:
---------
From: To:

Free Search:

Select Language version and font:
Enter search text:

Multilingual Scriptures Home » Swahili New Testament » 2 Timothy

Swahili New Testament
Chapter # Verse # Verse Detail
11Mimi Paulo, ambaye Mungu alitaka niwe mtume wa Kristo Yesu ili niutangaze ule uzima tulioahidiwa katika kuungana na Kristo Yesu,
12nakuandikia wewe mwanangu mpenzi Timotheo. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu.
13Ninamshukuru Mungu ambaye ninamtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya wazee wangu; namshukuru kila ninapokukumbuka daima katika sala zangu.
14Nakumbuka machozi yako na ninatamani usiku na mchana kukuona, ili nijazwe furaha.
15Naikumbuka imani yako ya kweli, imani aliyokuwa nayo nyanya yako Loisi, na pia mama yako Eunike. Nina hakika kwamba wewe pia unayo.
16Ndio maana nakukumbusha ukiweke motomoto kile kipaji ulichopewa na Mungu wakati nilipokuwekea mikono yangu.
17Kwa maana Mungu hakutupa Roho wa kutufanya tuwe waoga, bali alitupa Roho wa kutujalia nguvu, upendo na nidhamu.
18Basi, usione haya kumshuhudia Bwana wetu, wala usione haya kwa sababu yangu mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Lakini shiriki katika mateso kwa ajili ya Habari Njema, kadiri ya nguvu unazopewa na Mungu.
19Yeye alituokoa, akatuita tuwe watu wake yeye mwenyewe, si kwa sababu ya matendo yetu wenyewe bali kwa sababu ya kusudi lake na neema yake. Alitujalia neema hiyo katika Kristo Yesu kabla mwanzo wa nyakati;
110lakini sasa imefunuliwa kwetu kwa kuja kwake Mwokozi wetu Yesu Kristo. Yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Habari Njema akadhihirisha uzima usio kufa.
111Mungu amenichagua mimi niwe mtume na mwalimu kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema,
112nami nateseka mambo haya kwa sababu hiyo. Lakini niko bado timamu kabisa kwani namjua yule niliyemwamini, tena nina hakika kwamba yeye aweza kukilinda salama kile alichonikabidhi, mpaka Siku ile.
113Shika kwa makini mafundisho yale ya kweli niliyokufundisha, na kubaki katika hiyo imani na huo upendo wetu katika kuungana na Kristo Yesu.
114Jambo lile bora ulilokabidhiwa lilinde kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeishi ndani yetu.
115Kama unavyojua, watu wote mkoani Asia wameniacha, miongoni mwao wakiwa Fugelo na Hermogene.
116Bwana aihurumie jamaa ya Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha rohoni mara nyingi, wala hakuona haya kwa kuwa nilikuwa kifungoni,
117ila mara tu alipofika Roma, alianza kunitafuta kwa bidii mpaka akanipata.
118Bwana amjalie huruma katika Siku ile! Nawe wajua vizuri mengi aliyonifanyia huko Efeso.
21Basi, wewe mwanangu, uwe na nguvu katika neema tunayopata katika kuungana na Kristo Yesu.
22Chukua yale mafundisho uliyonisikia nikitangaza mbele ya mashahidi wengi, uyakabidhi kwa watu wanaoaminika, ambao wataweza kuwafundisha wengine pia.
23Shiriki katika mateso kama askari mwaminifu wa Kristo yesu.
24Mwanajeshi vitani hujiepusha na shughuli za maisha ya kawaida ili aweze kumpendeza mkuu wa jeshi.
25Mwanariadha yeyote hawezi kushinda na kupata zawadi ya ushindi kama asipozitii sheria za michezo.
26Mkulima ambaye amefanya kazi ngumu anastahili kupata sehemu ya kwanza ya mavuno.
27Fikiria hayo ninayosema, kwani Bwana atakuwezesha uyaelewe yote.
28Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa kutoka wafu, aliyekuwa wa ukoo wa Daudi, kama isemavyo Habari Njema ninayoihubiri.
29Kwa sababu ya kuihubiri Habari Njema mimi nateseka na nimefungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu haliwezi kufungwa minyororo,
210na hivyo navumilia kila kitu kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili wao pia wapate ukombozi upatikanao kwa njia ya Yesu Kristo, na ambao huleta utukufu wa milele.
211Usemi huu ni wa kweli: "Ikiwa tulikufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye.
212Tukiendelea kuvumilia, tutatawala pia pamoja naye. Tukimkana, naye pia atatukana.
213Tukikosa kuwa waaminifu, yeye hubaki mwaminifu daima, maana yeye hawezi kujikana mwenyewe."
214Basi, wakumbushe watu wako mambo haya, na kuwaonya mbele ya Mungu waache ubishi juu ya maneno. Ubishi huo haufai, ila huleta tu uharibifu mkuu kwa wale wanaousikia.
215Jitahidi kupata kibali kamili mbele ya Mungu kama mfanyakazi ambaye haoni haya juu ya kazi yake, na ambaye hufundisha sawa ule ujumbe wa kweli.
216Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ya kipumbavu; kwani hayo huzidi kuwatenga watu mbali na Mungu.
217Mafundisho ya aina hiyo ni kama donda linalokula mwili. Miongoni mwa hao waliofundisha hayo ni Humenayo na Fileto.
218Hawa wamepotoka kabisa mbali na ukweli, na wanatia imani ya watu wengine katika wasiwasi kwa kusema ati ufufuo wetu umekwisha fanyika.
219Lakini msingi thabiti uliowekwa na Mungu uko imara, na juu yake yameandikwa maneno haya: "Bwana anawafahamu wale walio wake," na "Kila asemaye yeye ni wa Bwana, ni lazima aachane na uovu."
220Katika nyumba kubwa kuna mabakuli na vyombo vya kila namna: vingine ni vya fedha na dhahabu, vingine vya mbao na udongo, vingine ni vya matumizi ya pekee na vingine kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
221Basi, kama mtu atajitakasa kwa kujitenga mbali na mambo hayo yote maovu, atakuwa chombo cha matumizi ya pekee, kwa sababu amewekwa wakfu, anamfaa Bwana wake na yupo tayari kwa kila kazi njema.
222Jiepushe na tamaa za ujana, fuata uadilifu, imani, upendo, amani, pamoja na watu wote ambao wanamwomba Bwana kwa moyo safi.
223Epuka ubishi wa kijinga na kipumbavu; wajua kwamba hayo huleta magomvi.
224Mtumishi wa Bwana asigombane. Anapaswa kuwa mpole kwa watu wote, mwalimu mwema na mvumilivu,
225ambaye ni mpole anapowaonya wapinzani wake, kwani huenda Mungu akawajalia nafasi ya kutubu, wakapata kuujua ukweli.
226Hapo fahamu zao zitawarudia tena, wakaponyoka katika mtego wa Ibilisi aliyewanasa na kuwafanya wayatii matakwa yake.
31Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu.
32watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu;
33watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema;
34watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu.
35Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo.
36Baadhi yao huenda katika nyumba za watu na huwateka wanawake dhaifu waliolemewa mizigo ya dhambi na ambao wanaongozwa na tamaa za kila aina;
37wanawake ambao wanajaribu daima kujifunza lakini hawawezi kuufikia ujuzi wa huo ukweli.
38Watu hao huupinga ukweli kama vile Yane na Yambre walivyompinga Mose.
39Lakini hawataweza kuendelea zaidi kwa maana upumbavu wao utaonekana wazi kwa wote. Ndivyo ilivyokuwa kwa akina Yane na Yambre.
310Wewe lakini, umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudi yangu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu, subira yangu,
311udhalimu na mateso yangu. Unayajua mambo yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Lustra. Nilivumilia udhalimu mkubwa mno! Lakini Bwana aliniokoa katika mambo hayo yote.
312Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe.
313Watu waovu na wadanyanyifu watazidi kuwa waovu zaidi na zaidi kwa kuwadanganya wengine na kudanganyika wao wenyewe.
314Lakini wewe dumu katika ukweli ule uliofundishwa, ukaukubali kabisa. Unawajua wale waliokuwa walimu wako.
315Unakumbuka kwamba tangu utoto wako umeyajua Maandiko Matakatifu ambayo yaweza kukupatia hekima iletayo wokovu kwa njia ya imani kwa Kristo Yesu.
316Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili,
317ili mtu anayemtumikia Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila tendo jema.
41Nakuamuru mbele ya Mungu, na mbele ya Kristo Yesu atakayewahukumu watu walio hai na wafu, na kwa sababu anakuja kutawala akiwa Mfalme:
42hubiri huo ujumbe, sisitiza kuutangaza (iwe ni wakati wa kufaa au wakati usiofaa), karipia, onya na himiza watu ukiwafundisha kwa uvumilivu wote.
43Utakuja wakati ambapo watu hawatasikiliza mafundisho ya kweli, ila watafuata tamaa zao wenyewe na kujikusanyia walimu tele watakaowaambia mambo yale tu ambayo masikio yao yako tayari kusikia.
44Watakataa kuusikia ukweli, watageukia hadithi za uongo.
45Wewe, lakini, uwe macho katika kila hali; vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Habari Njema, timiza kikamilifu utumishi wako.
46Kwa upande wangu mimi, niko karibu kabisa kutolewa dhabihu na wakati wa kufariki kwangu umefika.
47Nimefanya bidii katika mashindano, nimemaliza safari yote na imani nimeitunza.
48Na sasa imebakia tu kupewa tuzo la ushindi kwa maisha ya uadilifu, tuzo ambalo Bwana Hakimu wa haki, atanipa mimi Siku ile na wala si mimi tu, ila na wale wote wanaotazamia kwa upendo kutokea kwake.
49Fanya bidii kuja kwangu karibuni.
410Dema ameupenda ulimwengu huu akaniacha na kwenda zake Thesalonike. Kreske amekwenda Galatia, na Tito amekwenda Dalmatia.
411Luka peke yake ndiye aliye hapa pamoja nami. Mpate Marko uje naye, kwa maana ataweza kunisaidia katika kazi yangu.
412Nilimtuma Tukiko kule Efeso.
413Utakapokuja niletee koti langu nililoacha kwa Karpo kule Troa; niletee pia vile vitabu, na hasa vile vilivyotengenezwa kwa ngozi. ic
414Yule sonara aitwaye Aleksanda amenitendea maovu mengi; Bwana atamlipa kufuatana na hayo matendo yake.
415Jihadhari naye kwa sababu aliupinga ujumbe wetu kwa ukali.
416Wakati nilipojitetea kwa mara ya kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu; wote waliniacha. Mungu asiwahesabie kosa hilo!
417Lakini, Bwana alikaa pamoja nami, akanipa nguvu, hata nikaweza kuutangaza ujumbe wote, watu wa mataifa wausikie; tena nikaokolewa katika hukumu ya kifo kama kinywani mwa simba.
418Bwana ataniokoa na mambo yote maovu, na kunichukua salama mpaka katika Utawala wake wa mbinguni. Kwake uwe utukufu milele na milele! Amina.
419Wasalimu Priska na Akula, pamoja na jamaa ya Onesiforo.
420Erasto alibaki Korintho, naye Trofimo nilimwacha Mileto kwa sababu alikuwa mgonjwa.
421Fanya bidii kuja kabla ya majira ya baridi. Ebulo, Pude, Lino na Klaudia wanakusalimu; vilevile ndugu wengine wote.
422Bwana awe nawe rohoni mwako. Nawatakieni nyote neema.