Share this page:  
 

Multilingual Scriptures

(Compare books in 2 different language versions of your choice)

Comparison Search:

Select Language version and font:
You can only select max. of two versions.
Book:
Chapter:
Verse:
---------
From: To:

Free Search:

Select Language version and font:
Enter search text:

Multilingual Scriptures Home » Swahili New Testament » Colossians

Swahili New Testament
Chapter # Verse # Verse Detail
11Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo,
12tunawaandikia ninyi watu wa Mungu huko Kolosai, ndugu zetu waaminifu katika kuungana na Kristo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu.
13Daima tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, wakati tunapowaombea.
14Maana tumesikia juu ya imani yenu katika Kristo Yesu na juu ya upendo wenu kwa watu wote wa Mungu.
15Wakati ujumbe ule wa kweli, yaani Habari Njema, ilipowafikieni kwa mara ya kwanza, mlipata kusikia juu ya lile tumaini linalopatikana kwake. Kwa sababu hiyo imani na upendo wenu vinategemea jambo lile mnalotumainia ambalo mmewekewa salama mbinguni.
16Habari Njema inazidi kuzaa matunda na kuenea ulimwenguni kote kama vile ilivyofanya kwenu ninyi tangu siku ile mliposikia juu ya neema ya Mungu na kuitambua ilivyo kweli.
17Mlijifunza juu ya neema ya Mungu kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu, ambaye ni mfanyakazi mwaminifu wa Kristo kwa niaba yetu.
18Yeye alitupa habari za upendo wenu mliojaliwa na Roho.
19Kwa sababu hiyo tumekuwa tukiwaombeeni daima tangu tulipopata habari zenu. Tunamwomba Mungu awajazeni ujuzi kamili wa mapenzi yake, awajazeni hekima yote na elimu iletwayo na Roho wake.
110Hapo mtaweza kuishi kama anavyotaka Bwana na kutenda daima yanayompendeza. Maisha yenu yatakuwa yenye matunda ya kila namna ya matendo mema na mtazidi kukua katika kumjua Mungu.
111Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili mweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu.
112Na kwa furaha, mshukuruni Baba aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale Mungu aliyowawekea watu wake katika utawala wa mwanga.
113Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi,
114ambaye kwa njia yake tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa.
115Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana; ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.
116Maana kwa njia yake vitu vyote viliumbwa duniani na mbinguni, vitu vinavyoonekana na visivyoonekana: wenye enzi, watawala, wakuu na wenye mamlaka. Vyote viliumbwa kwa njia yake na kwa ajili yake.
117Kristo alikuwako kabla ya vitu vyote; kwa kuungana naye, vyote vyadumu mahali pake.
118Yeye ni kichwa cha mwili wake, yaani kanisa; yeye ni chanzo cha uhai wa huo mwili. Yeye ndiye mwanzo, mzaliwa wa kwanza aliyefufuliwa kutoka wafu, ili awe na nafasi ya kwanza katika vitu vyote.
119Maana Mungu alipenda utimilifu wote uwe ndani yake.
120Kwa njia yake Mungu alivipatanisha naye vitu vyote naam, viumbe vyote mbinguni na duniania; alileta amani kwa damu ya Kristo msalabani.
121Hapo kwanza ninyi pia mlikuwa mbali na Mungu na mlikuwa adui zake kwa sababu ya fikira zenu na matendo yenu maovu.
122Lakini sasa, kwa kifo cha Mwanae aliyeishi hapa duniani, Mungu amewapatanisha naye, kusudi awalete mbele yake mkiwa watakatifu, safi na bila lawama.
123Mnapaswa, lakini kuendelea kuwa imara na thabiti katika imani hiyo, na msikubali kusukumwa mbali na tumaini lile mlilopata wakati mlipoisikia Habari Njema. Mimi Paulo nimekuwa mtumishi wa hiyo Habari Njema ambayo imekwisha hubiriwa kila kiumbe duniani.
124Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani, nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, yaani kanisa.
125Nami nimefanywa kuwa mtumishi wa kanisa kufuatana na mpango wake Mungu ambao alinikabidhi kwa faida yenu. Mpango wenyewe ni kuutangaza kwa ukamilifu ujumbe wake,
126ambao ni siri aliyowaficha binadamu wote tangu milele, lakini sasa amewajulisha watu wake.
127Mpango wa Mungu ni kuwajulisha watu wake siri hii kuu na tukufu ambayo ni kwa ajili ya watu wote. Na, siri yenyewe ndiyo hii: Kristo yuko ndani yenu, na jambo hilo lamaanisha kwamba ninyi mtaushiriki utukufu wa Mungu.
128Kwa sababu hiyo tunamhubiri Kristo kwa watu wote; tunawaonya na kuwafundisha wote kwa hekima yote, ili tuweze kumleta kila mmoja mbele ya Mungu akiwa amekomaa katika kuungana na Kristo.
129Kwa madhumuni hayo mimi nafanya kazi na kujitahidi nikiitumia nguvu kuu ya Kristo ifanyayo kazi ndani yangu.
21Napenda mjue jinsi ninavyofanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, kwa ajili ya watu wa Laodikea na kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona kwa macho.
22Nafanya hivi kusudi mioyo yao ifarijiwe na kuvutwa pamoja katika upendo, ili wajazwe uthabiti mwingi uletwao na elimu ya kweli. Hapo wataijua siri ya Mungu ambayo ni Kristo mwenyewe.
23Ndani yake zimefichika hazina zote za hekima na elimu.
24Basi, nawaambieni, msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa maneno ya uongo hata kama ni ya kuvutia sana.
25Maana, ingawa mimi niko mbali nanyi kwa mwili, lakini niko pamoja nanyi kwa roho, na ninafurahi kuona uthabiti kamili mnaosimama nao pamoja katika imani yenu kwa Kristo.
26Maadamu ninyi mmemkubali Kristo Yesu kuwa Bwana, basi, ishini katika muungano naye.
27Mnapaswa kuwa na mizizi ndani yake, kujijenga juu yake na kuwa imara katika imani yenu kama mlivyofundishwa. Muwe na shukrani tele.
28Angalieni basi, mtu asiwapotoshe kwa udanganyifu mtupu wa hekima ya kibinadamu, ambayo chanzo chake ni mafundisho ya mapokeo ya watu na ya pepo watawala, na wala si Kristo mwenyewe!
29Maana, ndani yake Kristo katika ubinadamu wake, umo ukamilifu wote wa Mungu,
210nanyi mmepewa uzima kamili katika kuungana naye. Yeye yuko juu ya pepo watawala wote na wakuu wote.
211Katika kuungana na Kristo ninyi mlitahiriwa, lakini si kwa tohara ifanywayo na watu, bali inayofanywa na Kristo mwenyewe, na ambayo inahusikana na kukombolewa kutoka katika utu wa dhambi.
212Maana, mlipobatizwa mlizikwa pamoja na Kristo, na katika ubatizo, mlifufuliwa pia pamoja naye kwa imani yenu katika nguvu ya Mungu ambaye alimfufua Kristo kutoka wafu.
213Wakati mmoja nanyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu ninyi mlikuwa watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa ninyi uzima pamoja na Kristo. Mungu ametusamehe dhambi zetu zote;
214alifutilia mbali ile hati ya deni iliyokuwa inatukabili na masharti yake, na kuifuta kabisa kwa kuipigilia msalabani.
215Juu ya msalaba Kristo aliwapokonya nguvu zao hao pepo watawala na wakuu; aliwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuwaburuta kama mateka katika msafara wa ushindi wake.
216Kwa hiyo, basi, msikubali kupewa masharti na mtu yeyote kuhusu vyakula au vinywaji, siku za sherehe, sikukuu ya Mwezi mpya au Sabato.
217Mambo ya aina hiyo ni kivuli tu cha yale yatakayokuja; ukweli wenyewe ndiye Kristo.
218Msikubali kuhukumiwa na mtu yeyote anayejitakia kuwa wa maana kwa sababu ya maono ya pekee na ambaye anasisitiza juu ya unyenyekevu wa uongo na ibada kwa malaika. Mtu wa namna hiyo amepumbazika kwa fikira danganifu za kidunia
219na amejitenga na Kristo aliye kichwa cha huo mwili. Chini ya uongozi wa Kristo, mwili wote unalishwa na kuunganishwa pamoja kwa viungo na mishipa yake, nao hukua kama atakavyo Mungu.
220Ninyi mmekufa pamoja na Kristo na kukombolewa kutoka nguvu za pepo watawala wa ulimwengu. Kwa nini, basi, kuishi tena kama vile mngekuwa wa ulimwengu huu? Ya nini kuwekewa masharti:
221"Msishike hiki," "Msionje kile," "Msiguse kile!"
222Mambo hayo yote yanahusika na vitu vyenye kuharibika mara tu vinapotumiwa; hayo ni maagizo na mafundisho ya kibinadamu tu.
223Kweli, masharti hayo yaonekana kuwa ya hekima katika namna ya ibada ya kujitakia wenyewe, unyenyekevu wa uongo na kuutendea mwili kwa ukali; lakini kwa kweli, haifai chochote kuzuia tamaa za mwili.
31Basi, ikiwa mmefufuka pamoja na Kristo, panieni mambo ya juu, kule Kristo aliko, ameketi upande wa kulia wa Mungu.
32Muwe na hamu ya mambo ya huko juu, na siyo mambo ya hapa duniani.
33Maana ninyi mmekufa na uzima wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.
34Uzima wenu halisi ni Kristo, na wakati atakapotokea ndipo nanyi pia mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.
35Basi, komesheni kabisa kila kitu kilicho ndani yenu ambacho chahusika na mambo ya kidunia: uasherati, uchafu, shauku, tamaa mbaya na uchu (ambao ni sawa na kuabudu sanamu).
36Kwa sababu ya mambo hayo hasira ya Mungu huwajia wote wanaomwasi.
37Wakati mmoja ninyi pia mliishi kufuatana na mambo hayo, mlipotawaliwa nayo.
38Lakini sasa mnapaswa kuachana na mambo haya yote: hasira, tamaa, uovu; kufuru au maneno yasiyofaa yasitoke kamwe vinywani mwenu.
39Msiambiane uongo, kwani ninyi mmekwisha vua ule utu wa kale pamoja na matendo yake yote,
310mkavaa utu mpya. Huu unaendelea kurekebishwa na Mungu, Muumba wake, kadiri ya mfano wake, ili mpate kumjua Mungu kwa ukamilifu.
311Katika hali hii, hakuna tena tofauti kati ya Mgiriki na Myahudi, aliyetahiriwa na asiyetahiriwa, msomi na asiye msomi, mtumwa na mtu aliye huru. Kristo ni kila kitu, na yumo katika yote.
312Ninyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu.
313Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe ninyi.
314Zaidi ya hayo yote, zingatieni upendo kwani upendo huunganisha kila kitu katika umoja ulio kamili.
315Nayo amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu; maana kwa ajili hiyo ninyi mmeitwa katika mwili huo mmoja. Tena muwe na shukrani!
316Ujumbe wa Kristo ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani.
317Na, kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa jina la Bwana Yesu na kumshukuru Mungu Baba kwa njia yake.
318Enyi akina mama, watiini waume zenu, kwani ndivyo apendavyo Bwana.
319Nanyi waume, wapendeni wake zenu, na msiwe wakali kwao.
320Enyi watoto, watiini wazazi wenu daima maana hiyo humpendeza Bwana.
321Nanyi wazazi, msiwachukize watoto wenu, la sivyo watakata tamaa.
322Enyi watumwa, watiini wakuu wenu wa kidunia katika mambo yote, na si tu wakati wanapowatazama kwa kuwa mnataka kujipendekeza kwao; ila fanyeni hivyo kwa moyo wote, kwa sababu ya kumcha Bwana.
323Kila mfanyalo, fanyeni kwa moyo wote, kwa sababu ya Bwana na si kwa ajili ya mtu.
324Kumbukeni kwamba atawapeni tuzo lile alilowawekea watu wake. Mtumikieni Kristo Bwana!
325Atendaye mabaya atalipwa kufuatana na ubaya wake; Mungu hana ubaguzi.
41Nanyi wakuu, watendeeni watumwa wenu kwa uadilifu na haki, mkikumbuka kwamba nanyi pia mnaye Bwana mbinguni.
42Dumuni katika sala, na mnaposali muwe waangalifu, mkimshukuru Mungu.
43Vilevile, mtuombee sisi pia ili Mungu atupe fursa ya kuuhubiri ujumbe wake kuhusu siri ya Kristo. Kwa ajili hiyo mimi niko sasa kifungoni.
44Basi, ombeni ili niweze kusema kama inavyonipasa na kwa namna itakayodhihirisha siri hiyo.
45Muwe na hekima katika uhusiano wenu na watu wasioamini, mkitumia vizuri kila nafasi mliyo nayo.
46Mazungumzo yenu yanapaswa kuwa daima mema na ya kuvutia, na mnapaswa kujua jinsi ya kumjibu vizuri kila mmoja.
47Ndugu yetu mpenzi Tukiko, mfanyakazi mwaminifu na mtumishi mwenzetu katika kazi ya Bwana, atawapeni habari zangu zote.
48Ndiyo maana namtuma, ili aichangamshe mioyo yenu kwa kuwaambieni habari zetu.
49Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpenzi na mwaminifu, ambaye ni mwananchi mwenzenu. Watawapeni habari za mambo yote yanayofanyika hapa.
410Aristarko, ambaye yuko kifungoni pamoja nami, anawasalimuni; hali kadhalika Marko, binamu yake Barnaba, (mmekwisha pata maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni).
411Naye Yoshua aitwaye Yusto, anawasalimuni. Miongoni mwa Wayahudi waliokwisha pokea imani, hawa tu peke yao, ndio wanaofanya kazi pamoja nami kwa ajili ya Utawala wa Mungu; nao wamekuwa msaada mkubwa kwangu.
412Epafra, mwananchi mwenzenu na mtumishi wa Kristo Yesu anawasalimuni. Daima anawaombeeni ninyi kwa bidii ili mpate kusimama imara, mkomae na kuwa thabiti kabisa katika mambo yote anayotaka Mungu.
413Naweza kushuhudia kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu na kwa ajili ya watu wa Laodikea na Hierapoli.
414Luka, daktari wetu mpenzi, na Dema, wanawasalimuni.
415Salamu zetu kwa ndugu zetu wa Laodikea; msalimuni dada Nimfa pamoja na jumuiya yote ya waumini inayokutana nyumbani kwake.
416Mkisha soma barua hii, hakikisheni kwamba inasomwa na Wakristo wa Laodikea; na ninyi fanyeni mpango mpate kuisoma barua waliyoipata kwao.
417Mwambieni Arkipo aitekeleze vizuri ile huduma aliyokabidhiwa na Bwana.
418Naandika haya kwa mkono wangu mwenyewe: Salamu kutoka kwangu, mimi Paulo. Kumbukeni kwamba niko kifungoni. Neema ya Mungu iwe nanyi.